Mahakama ya Southward Crown ambako kesi inaunguruma.
MTAALAM wa sayansi katika moja ya taasisi maarufu za utafiti duniani nchini Uingereza anakabiliwa na mashitaka ya kumchukua msichana kutoka Tanzania na kukaa naye nyumbani kwake akimfanyisha kazi za kitumwa.
Kwa mujibu wa gazeti la Daily Mail, mwana mama Rebecca Balira mwenye umri wa miaka 47 (pichani juu) anatuhumiwa kumfanyia unyama huo Mtanzania Methodia Mathias (21) ambaye anamfanyisha kazi za kupika, kufua na kufanya usafi nyumbani kwake huku akimtumia kama yaya wa watoto wake watatu, bila ya kumlipa ujira wowote, imeambiwa mahakama ya Southward Crown, jijini London.
Msichana huyo ambaye alisafirishwa na Balira kutoka Tanzanzania hadi Uingereza, huamka saa 11 asubuhi ambapo hufanyishwa kazi hadi saa 5:30 za usiku au hadi usiku wa manane, mahakama imeambiwa na kuelezwa zaidi kwamba msichana huyo hulazimishwa kutumia kitanda kimoja na mtoto wa kiume Balira mwenye umri wa miaka 12.
Katika mazingira hayo hayo magumu, Mathias amenyang’anywa pasipoti yake na haruhusiwi kuongea na mtu yeyote, achilia mbali mateso ya kupigwa na “tajiri” wake huyo ambapo katika tukio moja aliwahi kumjeruhi na mkasi kifuani.
Mateso hayo ambayo yalimchukua muda wa miezi sita yalifikia kikomo baada ya msichana huyo kumweleza ‘rafiki’ yake mmoja nchini humo mkasa huo naye akamshauri kuuripoti polisi ambao walifika na kuanza upelelezi.
Mwendesha mashitaka, Caroline Haughey aliiambia mahakama jinsi Balira alivyokuwa amemwahidi Mathias kumlipa mshahara wa shilingi 250,000 za Kitanzania kila mwezi (kiasi cha Pauni 96) ili kwenda kumfanyia kazi za ndani.
Balira alifanikiwa kumsafirisha msichana huyo kutoka Dar es Salaam hadi London, kupitia Taasisi ya Utafiti wa Dawa za Tropiki ya London ambapo alimpeleka huko Februari mwaka jana (2010) katika fleti la vyumba viwili vya kulala huko Thamesmead, kusini-mashariki mwa London ambako Balira alikuwa akitumia chumba kimoja na watoto wake watatu na kimoja kukipangisha kwa mtu mwingine.
Mbali na kutolipwa ujira anaostahili, msichana huyo alikuwa hatoki nyumbani hapo isipokuwa Jumapili tu wakati wanakwenda kanisani. Imeelezwa pia kuwa alikuwa akilipwa pauni 96 tu, takribani 250,000 za bongo kwa mwezi.
Wakati kesi hiyo ikiendelea katika mahakama hiyo, upande wa mashitaka umesema kwamba:
“Tunachokisema ni kwamba Rebecca Balira alimfanya Methodia Mathias kuishi katika mazingira ambayo ni sawa kabisa na utumwa.”
Kesi hiyo inaendelea ambapo Balira anakabiliwa na mashitaka ya kuendesha utumwa na mashambulio mawili ya mwili.
source: global publishers
No comments:
Post a Comment